TAARIFA MUHIMU :

KAZI ZA BAKIZA


Bakiza lina kazi nyingi ambazo zinajiegemeza katika maeneo muhimu yafuatayo:-

  • Uelimishaji:

Kutoa taaluma kwa jamii juu ya matumizi sahihi, fasaha na sanifu ya Kiswahili katika taasisi za umma na binafsi kupitia vipindi vya redio, televisheni na makala katika majarida na magazeti. Kuandaa na kuendesha mafunzo, mijadala, midahalo, makongamano na semina kwa lengo la kuwajengea uwezo walimu, wanafunzi, wanahabari na wadau wengine wa Kiswahili na kupata fursa ya kujadili na kubadilishana mawazo kitaaluma.

  • Uhariri:

Kuhariri miswada ya vitabu vya Kiswahili na nyaraka nyengine kutoka taasisi na watu binafsi na kutoa ithibati juu ya usahihi wa lugha iliyotumika

  • Usanifishaji:

Kwa kushirikiana na taasisi nyengine kutafsiri na kuandaa istilahi zinazofaa kutumika katika nyanja mbalimbali za kitaaluma.

  • Ushajiishaji:

Kuandaa mashindano ya uandishi kwa wanafunzi, waandishi na watunzi wa vitabu chipukizi na mahiri ili kuwashajiisha kutunga na kuandika kazi zenye ubora.

  • Uchapishaji:

Kutoa machapisho ya Baraza kama vile majarida, makamusi, makala, vitabu, vipeperushi na miongozo mengingine kwa lengo la kuendeleza Kiswahili.

  • Utafiti:

Kwa kushirikiana na wana taaluma, wazawa na weledi wa lugha ya Kiswahili, kufanya utafiti juu ya masuala mbalimbali ya fasihi na isimu ya lugha, kuyaandikia makala na hatimaye kuyachapisha vitabu.

  • Huduma za Tafsiri:

Kutafsiri kazi kama vile nyaraka, miswada, makala au sera kutoka Serikalini, taasisi mbalimbali na watu binafsi zinazohtaji kutafsiriwa kutoka Kiswahili kwenda lugha nyengine na kutoka lugha nyengine kwenda Kiswahili; pamoja na kutoa ithibati kwa kazi iliyotafsiriwa nje ya BAKIZA. Aidha, Baraza linatoa huduma ya ushauri kwa waandishi wa vitabu pamoja na uhariri wa miswada ya vitabu vya Kiswahili kabla ya kuchapishwa.

  • Huduma za Maktaba:

Kwa sasa BAKIZA ina maktaba ndogo yenye vitabu vizuri na muhimu vinavyowafaa walimu, wanafunzi wa skuli za msingi, sekondari na hata vyuo. Huduma hii hutolewa siku zote za kazi.

MATANGAZO