BAKIZA

HISTORIA YA BARAZA

  •   HISTORIA KABLA YA MAPINDUZI

Kabla ya Mapinduzi ya Januari 1964 shughuli za kusimamia lugha ya Kiswahili zilikuwa chini ya Kamati ya Lugha ya Kiswahili ya Afrika Mashariki (The Interterritorial Swahili Language Committiee) iliyoanzishwa mwaka 1930. Kamati hii ilifanya kazi kwa kipindi cha miaka 34 na ilikuwa na utaratibu wa kupokezana Makao Makuu yake miongoni mwa nchi wanachama. Kazi kubwa zilizofanywa na Kamati hiyo ni pamoja na:-

Usanifishaji wa lahaja ya Kiunguja Mjini ili iwiane katika msamiati, sarufi na maandishi kwa lengo la kutumika katika mawasiliano rasmi ya kitaasisi na serikali ndani ya nchi wanachama za Afrika Mashariki.

Mwaka 1930-1942 ilifanya urekebishaji wa Kamusi ya Madan la Kiingereza/Kiswahili.

Mwaka 1933-1039 iliimarisha makamusi yalilotayarishwa na Frederic Johnson ya Kiingereza/Kiswahili na Kiswahili/Kiingereza, makamusi ambayo yamesaidia sana walimu, wanafunzi, wataalamu na watafiti kupata marejeo ya kukamilisha kazi zao.

Kutoa vijarida mia sita kila mwaka vinavyoelezea mada za kiisimu kama vile maumbo sanifu, vipengele vya sarufi, maneno mapya na matokeo ya tafiti za Kiswahili.

Kuandika vitabu vya matokeo ya utafiti wa lahaja za Kiswahili zinazozungumzwa Zanzibar na Mombasa.

Hata hivyo kazi nzuri ilikuwa ikifanywa na watunzi na waandishi wa vitabu kuiendeleza lugha ya Kiswahili, kwani wao walibeba dhima ya kufunza, kuonya, kuasa na kuburudisha kupitia kazi zao za sanaa zilizosarifiwa kwa lugha sahihi, fasaha, yenye mvuto na isiyoleta karaha wala utusani inapotumika mbele ya hadhara.

Kupitia Wizara ya Elimu hatua za kuziba pengo la ukosefu wa vitabu vya kusomeshea ilichukuliwa, hivyo kufanya kazi kubwa ya kukihami Kiswahili kwa kuandika vitabu kama vile Kiswahili Lugha Yetu na Someni kwa Furaha, ambavyo vilitumika kusomeshea madarasa ya msingi. Vitabu hivyo vilivyoandikwa na wazalendo vilihifadhi taaluma ya lugha ya Kiswahili iliyofungamana na mila, silka, tamaduni na mazingira halisi yanayoizunguka jamii ya wanafunzi.

  •   HISTORIA BAADA YA MAPINDUZI

Katika mwaka 1983 chombo rasmi cha serikali cha kusimamia lugha ya Kiswahili; matumizi na maendeleo yake kilianzishwa kwa sheria namba 7 ya mwaka 1983. Chombo hicho kiliitwa Baraza la Taifa la Kiswahili la Zanzibar. Hata hivyo, utendaji wa shughuli za Baraza hili haukuwa katika kasi iliyotarajiwa kutokana na kukosa ofisi za kufanyia kazi, kutokuwa na watendaji walioajiriwa na bajeti finyu iliyokuwa ikitengwa na kutumika kwa shughuli nyengine za wizara.

Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) liliasisiwa kwa sheria namba 4 ya Baraza la Wawakilishi la Zanzibar ya mwaka 2004. Baraza lilianzia likiwa chini ya Wizara ya Elimu, Utamaduni na Michezo, baadaye Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo na hata baada ya wizara kuongezewa jukumu la utalii na kuwa chini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Utalii ya Michezo na hivi sasa Baraza lipo chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibzr. Chombo hiki kimeundwa kwa madhumuni ya kusimamia masuala yote yanayohusu lugha ya Kiswahili, matumizi, maendeleo, mafanikio na changamoto zake Zanzibar.