BWANA HAJI GORA HAJI
Uzawa wa Haji Gora ulitokea mwaka 1933 katika Kisiwa cha kale cha kihistoria cha Tumbatu kilichopo Kaskazini ya Unguja.
Mwana kindakindaki huyu wa Tumbatu anatokana na ukoo wa masikini wa watoto sita kwa upande wa mama mmoja na baba mmoja.
Anao ndugu wanne wa mama mmoja na baba mbalimbali. Amepata elimu ya madrasa mjini Unguja kwa Bi. Mwanadarini katika mtaa wa Vuga.
Alimaliza elimu ya Qur' an katika madrasa ya Maalim Ibrahim Juma Ngwali Kisiwani Tumbatu.
Mazingira ya kisiwa cha Tumbatu ni ya shughuli za uvuvi na utwesi wa majahazi ya kusafiria. Mapema ya alfajiri ya maisha yake katika umri wa
miaka minane aliabiri vyomboni. Humo alivua maji mafu na bahari kuu. Akitoka chombo hiki hupanda kile katika madau na ngalawa.
Alipochuchuka akajihaulisha katika majahazi na kusafiri bahari kuu katika mwambao wote wa Afrika ya Mashariki. Huko alipanda daraja baada ya
daraja ya uledi, sarahangi hadi unahodha. Utwesi wa bahari kuu ulimfungua macho na kuijua dunia. Ubaharia na uvuvi alipoupa kichogo, ukuli wa
bandarini Unguja ukampungia mkono kumwita naye akaukumbatia. Kazi zote hizo za sulubu hazikumpa tijara zaidi ya kumkongeresha.
Jahazi lake la safari ndefu ya ndoa iling'oa nanga katika mapambazuko ya mwaka 1950 akiwa barubaru wa miaka kumi na saba. Katika nyakati tofauti
alioa na kuacha. Alioa sanjari wakeze wafuatao: Bi. Mlisho Pandu Kombo, Bi. Bahati Makame Kombo, Bi. Sepia Musa Kombo, Bi. Maliza Ngwali Khamis
na Bi. Patima Pandu Mdungi. Wake wote hao amezaa nao ukiacha Bi. Sepia Musa. Jumla ya watoto wake ni kumi na saba.
Usanii kipawa, kilichoteka huba za wengi kilichomoza mapema katika ujana wake. Akiwa Tumbatu alijiunga na kikundi cha sanaa kilichojulikana kwa
jina la Zige, kikundi cha tambo na malumbano kishairi dhidi ya Kaza Roho. Wakati Watumbatu wakivutiwa na malumbano ya Haji Gora na mpinzani wake,
kikundi cha ngoma cha Ujinga Mwingi kikamvuta Haji Gora na huko aliziteka nyoyo na hisia za washabiki. Huko akalumbana na Makame Kitenge kwa
usogora na kughani.
Mwaka 1957 msanii huyu akahamia mjini akiwa mshairi, mpiga ngoma na mtambaji katika kughani nyimbo. Mji ukamkubali. Sanaa ya Taarab asilia ikamteka
na kujiunga na vikundi vya Taarab kimoja baada ya kimoja. Alianza Michenzani, akaenda Mlandege, na hatimaye 'Culture'. Katika vikundi hivyo alikutana
na washairi wabobevu kama Hoja Saleh na Bai Muhamed. Waimbaji wenye majina kama Bakari Abeid, Salim Kasim na Seif Salim. Nyimbo zake darzeni kadhaa
ziligombaniwa na kuimbwa zikiwemo Kitendawili, Mpewa Hapokonyeki, Usimpige Mke na Dunia ni Rangi Mbili.
Utunzi wa vitabu Kimbunga, Malenga wa Tumbatu na Kamusi ya Kitumbatu ndiyo ulohitimisha usanii wake kwa vitabu. Ametunukiwa vyeti na tunuku nyingi na
asasi kadhaa kutokana na umahiri wake wa utunzi wa ushairi na ufasaha wa lugha. Aidha, baadhi ya mashairi yake yametafsiriwa kwa lugha ya Kifaransa na
Issa Pascal Bacuez.
Haji Gora ni msanii aliyejibadilisha mwenyewe kisanaa akiziteka nyoyo za wengi na kujiwekea jukwaa la kisanaa la umaarufu Zanzibar na ulimwenguni.