BWANA MUHAMED SAID ABDALLA (BWANA MSA)
Jina lake halisi la mwandishi wa riwaya za upelelezi za Kiswahili ni Muhamed mtoto wa Said mjukuu wa Abdulla. Herufi tatu za awali za majina yake yanaunda
jina lake maarufu la Bwana MSA. Jina hili ndilo la mhusika wake katika riwaya zake sote. Uzawa wake ulitokea nje ya mji wa Zanzibar ktika kijiji cha Makunduchi,
tarehe 25 Aprili, 1918, Muhamed alizaliwa. Aliishi miaka themanini na tatu na kufariki mwezi Machi mwaka 1991. Alioa na kuzaa watoto watatu, wawili wakike mmoja
wa kiume aliyekuwa mwimbaji mzuri wa taarabu hasa kwa nyimbo Kiarabu.
Alisoma Skuli ya msingi mwaka 1928 na baadaye Sekondari katika skuli ya Kikiristo ya Kiungani na kumaliza mwaka 1938. Ingawa wakati huo kulikuwa hakuna Chuo cha
Uandishi wa habari, Bwana MSA tangu mapema aliipenda kazi hiyo na kuseleleya nayo. Katika ujana na ubichi wa umri wake aliajiriwa na kupewa jukumu la kuwa Mhariri..
Aidha katika nyakati tofauti alikuwa Mhariri wa magazeti ya Mkulima Zanzibar, Al-Falak, Afrika Kwetu na Al-Mahida. Pia wakati fulani alifanya kipindi kilichokuwa maarufu
sana katika radio ya sauti ya Unguja kikiitwa “Sadiki Ukipenda”. Hamu na shauku ya kutaka kuandika riwaya badala ya uhariri wa magazeti ikampamba. Wakati ule Lujna ya Afrika
ya Mashariki ikahimiza waandishi chipukizi kushindana katika kuandika kazi za riwaya. Mwaka 1958 fursa ikatokea na yeye hakufanya ajizi akajitosa katika mashindano ya uandishi wa
riwaya kwa wananchi wa Zanzibar, Tanganyika, Uganda na Kenya.
Riwaya yake ya Mzimu wa watu wa kale ikazipiku kazi zote na kushinda. Kuanzia hapo kazi za riwaya za upelelezi zilizochorwa katika mazingira ya Kiswahili ya uhalisia wa Zanzibar
zikapata umaarufu na kulitawala soko la Riwaya za Kiswahili. Moja ya sifa ya Bwana MSA ni uhodari wa kuunda wahusika wake na kuibua taharuki.
Muhamed Said Abdalla (MSA) alitunga hadithi fupifupi na riwaya. Riwaya hizo ni pamoja na Mzimu wa watu wa kale (1966), Kisima cha Gingingi (1968), Duniani kuna Watu (1973), Siri
ya sufuri (1977), Mke mmoja Waume watatu (1975), Mwana wa Yungi Hulewa (1976) na Kosa la Bwana Msa (1984). Katika uhai wake ameandika riwaya za upelelezi kwa uhodari mkubwa.
Waandishi wengi wa Zanzibar wa riwaya za Kiswahili kina Said Ahmed, Muhamed Suleiman na Adam Shafi wamemvulia kofia kwa ubingwa na wanakiri kuwa riwaya zake ndizo
zilizowaraghabisha kupenda kuandika.