BAKIZA

DKT. MUHAMMED SEIF KHATIB

Umbuji ni kijiji kiliopo pembezoni mwa Wilaya ya Kati, uzawa wa Muhammed Seif Khatib ulitokea usiku wa manane wa tarehe 10 Mei, 1952, majira ya vuli. Kiuzawa, ubabani anatoka kwenye ukoo wenye asili ya kusini ya Makunduchi na Jambiani. Ndoa ya baba mzazi Seif Khatib na mama mzazi Tatu Kombo ilibarikiwa watoto wanne, wanawake wawili na wanaume wawili; Sijamini, Ali, Muhammed (marehemu)na kitindamimba Maimuna (marehemu). Bwana Seif alioa mke mwengine na kubarikiwa mtoto mwanamke aitwaye Rukia (marehemu).


Mwandishi huyu ingawa alizaliwa kijijini lakini makuzi yake yalifinyangwa mjini. Alipata elimu yake ya Madrasa katika chuo cha Bi. Mwanzena na badaye kidogo Msikiti Barza. Elimu ya msingi alisoma Fuoni na Kiembesamaki. Hakufaulu kwenda sekondari. Alisomea Ualimu Nkrumah na kufundisha skuli kadhaa za msingi ikiwemo Umbuji, Chaani, Darajani na Forodhani. Muhammed muda wote hakutosheka na kiwango chake cha elimu. Alihangaika huku na huku, panda shuka hadi pale alipofanikiwa kuhitimu elimu ya sekondari ya kiwango cha kawaida na kuwa mtahiniwa wa faragha kwa sekondari ya kiwango cha juu. Baadaye akajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1975. Baada ya kusomesha muda mfupi Chuo cha Uwalimu na taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni, Muhammed alibahatika kwenda Uingereza kuchukua shahada ya uzamili katika skuli ya School of Oriental and African Study ya Chuo Kikuu cha London mwaka 1981/2. Shahada ya uzamivu aliipata Chuo Kikuu cha Dodoma.


Ajali ya maisha ilitokea na akajikuta ameingia katika siasa za vijana kwa miaka 10 (1978 - 1988). Miaka 23 iliyofuatia (1988 - 2010) akahudumu katika Serikali akiwa waziri wa mambo ya ndani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ofisi ya Waziri Mkuu - Habari na Siasa na baadae kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo. Pia aliwahi kujiunga katika nafasi za ubunge wa vijana na hatimaye kuwa mbunge wa jimbo la Uzini hadi 2015.


Kipaji cha usanii cha Muhammed kilihitaji kuibuliwa. Alikuwa mshiriki wa sanaa za mashairi tokea yupo skuli za msingi na kuwahi kutunga mashairi na kusomwa sauti Unguja kwa wakati huo na sasa ni Redio ya Shirika la Utangazaji la Zanzibar (ZBC). Alipokuwa chuo cha Uwalimu alitunga mashairi ya nyimbo, kuweka sauti na hata kuimba Taarab asilia. Ushiriki wake katika vikundi vya Taarab ya Kikwajuni na Nadi Akhwani - Safaa kulipalilia kumea kwa kipawa cha ushairi. Kazi yake ya kwanza iliyochapishwa ilikuwa ni Utenzi wa Ukombozi wa Zanzibar (1975) ikafuatia na Fungate ya Uhuru (1988), Pambazuko la Afrika (1982), Kipanga (Hadithi Fupi), Taarab Zanzibar (1992), Wasakatonge (2016), Chanjo (2016) na Vifaru Weusi (2016).

Kudumu kwa kazi ya Fungate ya Uhuru na Wasakatonge katika utahini wa sekondari nchini Tanzania ni uthibitisho wa kazi nzuri sana ya ushairi wake. Kazi mbili hizi zilipata tunzo, Fungate ya Uhuru ilipata tunzo ya Shaaban Robert iliyotolewa na BAKITA na Wasakatonge iliyotolewa na PATA (Jumuiya ya Uchapishaji Tanzania).


Dkt. Seif pia alikuwa ni mhadhiri wa vyuo mbalimbali nchini Tanzania na Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) hadi umauti wake ulipomkuta mwaka 2020.


MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU PEPONI - AMIN