BAKIZA

PROFESA SAID AHMED MOHAMED

Said Ahmed Mohamed mwaka 1947 alizaliwa katika mtaa wa Limbani, Wete Pemba tarehe 12 Disemba. Utoto wake ulikuzwa na kuengwaengwa Kisiwani Unguja ambako alisoma juzuu na Mas-haf katika madrasa na kuidhinishwa kusoma Qur an. Skuli ya Darajani iliyopo mpakani kati ya ng'ambo na Mji Mkongwe aliweka unyayo wake katika safari ndefu ya kuisaka elimu . Ufaulu wake ulimpeleka skuli ya sekondari iliyokuwa ikiitwa King George VI.


Mwaka 1966 alijunga na Chuo cha Uwalimu Nkrumah. Kati ya mwaka 1969 na 1974 akaajiriwa na kuanza kufundisha skuli tafauti kisiwani Pemba. Said alifundisha masomo ya Sayansi na hesabu na sio lugha. Hamu ya kujiendeleza kielimu ikamsukuma na kujiandaa. Mwaka 1976 alitahamaki yupo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anachukua masomo ya Kiswahili, Fasihi na Isimu, Fasihi kwa Kiingereza na Ualimu. Matokeo mazuri sana ya masomo ya shahada ya kwanza yaliwavutia walimu wake. Mhadhiri Sigmund Brunner kutoka Ujerumani Mashariki aligundua mapema kipaji chake na kumshawishi aende Ujerumani kwa masomo ya juu. Bila zohali wala ajizi, Salim akajiabiri katika ndege hadi Ujerumani na kujiunga na Chuo Kikuu cha Kirl Marx hapo Leipzig mwaka 1985.


Said alikuwa mwanafunzi wa Isimu na wakati huo huo mwalimu wa Kiswahili kwa Wajarumani wasomao Kiswahili. Shahada za umahiri na Uzamivu akazikamilisha kwa kiwango cha kuridhisha. Akarudi nyumbani na kuanza kufundisha katika vyuo mbalimbali. Aliwahi kuwa mkurugenzi wa iliyokuwa Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni (TAKILUKI). Taaluma yake ya kufundisha na umahiri wake wa kuandika ukawa chagizo kwake. Vyuo na asasi za elimu zikawa zinapigana vikumbo kumwinda. Said alifundisha Nairobi, Kenya na baadaye Japan, Osaka ambako alitunukiwa Uprofesa kabla kuhitimisha kufundisha huko Ujerumani katika Chuo Kikuu cha Bayreuth mwaka 1992. Hivi sasa amestaafu lakini Waswahili husema ujuzi hauzeeki. Chuo Kikuu cha Zanzibar kimemuomba afundishe kozi za Uzamivu..


Kipaji chake cha uandishi ni cha urithi wa mama yake ambaye alikuwa mtunzi wa nyimbo za papo kwa papo na mghani mashuhuri na mtambaji wa hadithi za Fasihi Simulizi.

Mkaa na waridi haachi kunukia, Said alipata majazi ya mama tokea utotoni. Akiwa shuleni darasa la tano alianza kutunga hadithi na mashauri, mambo yaliyowavutia sana walimu wake. Shairi lililovutia zaidi ni like liitwalo 'Nimfuge Ndege Gani?' (1960) kuanzia hapo kalamu hakuiweka chini. Akaandika mashairi yaliyosomwa katika redio ya sauti ya Unguja siku hizo na sasa ni redio ya Shirika la Utangazi la Zanzibar (ZBC). Alitiwa moyo na kuraghabishwa na jozi ya walimu wake Mohamed Abdulla na Kindy Abubakar.


Mwandishi huyu alikuwa mchanga alianza kunyemelewa na umaarufu pale hadithi zake fupi zilipoanzwa kusomwa katika idhaa ya BBC na DW. Kuanzia mwaka 1976 kilipotoka kwa kishindo kitabu chake cha kwanza cha riwaya ya Asali Chungu hadi sasa ameandika jumla ya vitabu sitini na saba vikiwemo riwaya, Hadithi fupi, mashairi na heshima za lugha na Isimu. Vitabu vya hivi karibuni ni Babu Alipofufuka (2001), Dunia Yao (2006), Nyuso za Mwanamke (2010), Atamlilia Nani (2009), Vipawa vya Hasina (2009), Mkama Ndume (2013), Masikini Bibi Yangu (2009), Kimya Kimya, Mshetani Wamerudi. Riwaya hizi zina mwelekeo mpya wa usasa baadaye tofauti na riwaya kabla ya hizi. Riwaya na kazi nyengine za fasihi ni pamoja na Sikate Tamaa (2001), Kina cha Maisha (1984) na Jicho la Ndani (2000). Riwaya zake nyingine ni Posa za Bi Kisiwa (2007), Asali Chungu (1977), Dunia Mti Mkavu (1980), Kiza katika Nuru (1988) na Tata za Asumin (1990).


Said Ahmed Muhamed ni mwandishi mwenye kipaji cha kipekee sio cha kuweza kuandika kazi nyingi zenye viwango tu bali kuweza kuziandikia tanzu zote tatu za fasihi; ushairi, tamthilia na riwaya. Jina lake linavuma na kazi zake zinatamba nje na ndani ya Afrika Mashariki. Mchango wake katika uwanja wa Fasihi ya Kiswahili hauna kadiri. Ni mwana isimu, Profesa na mwandishi mwenye kipaji cha kipekee cha uandishi anayepasa kutambuliwa na kuenziwa.