PROFESA MOHAMED ABDULLA MOHAMED
Prof. Mohamed Abdulla Mohamed alizaliwa katika kisiwa cha Unguja mwaka 1941. Alipata elimu yake ya msingi na sekondari Unguja baina ya mwaka
1952 -196. Mwaka 1963 alihitimu shahada ya ualimu katika Chuo cha Ualimu cha Dar es Salaam. Baada ya hapo alijiunga na Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam ambako alitunukiwa Shahada ya Sanaa mwaka 1973. Baada ya kutunukiwa shahada hiyo, alijiunga tena na masomo ya Shahada ya Uzamili
ya Sanaa katika Elimu ambapo alihitimu mwaka 1975. Baada ya hapo aliendelea na masomo ya Uzamili katika Chuo Kikuu cha Colombia (Marekani) ambako
mwaka 1983 alihitimu shahada ya Uzamili katika Isimu Tumikizi (Applied Linguistics). Shahada nyengine aliyopata ni shahada ya Uzamili katika
Sayansi (MSc) katika Chuo Kikuu cha New York mwaka 1986.
Prof. Mohamed aliwahi kufanya kazi kama vile Mkaguzi wa Vyama vya Ushirika Tanzania mwaka 1962 - 1969. Baadaye, alifanya kazi ya kufundisha katika
Skuli za Sekondari za Tanzania, akisomesha masomo ya Kiingereza, Kiswahili, Hisabati na Historia. Baada ya masomo yake, kuanzia 1981/1982 alifanya
kazi katoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kama Mtafiti mwandamizi na Mhadhiri. Aidha, akiwa masomoni katika Chuo Kikuu cha Colombia mwaka 1983 - 1986
alifanya kazi ya kufundisha kwa muda maalumu katika Chuo Kikuu hicho cha Colombia na vyuo vyengine mbalimbali kama vile The Hunter College of the City,
University and the York University in the United Kingdom akiwa profesa msaidizi.
Mwaka 1986/1987 alikuwa Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alifundisha Isimu ya Kiswahili. Mwaka 1988 - 1990 alifanya kazi katika Chuo Kikuu
cha Moi nchini Kenya kama Profesa mshiriki katika Skuli ya Taaluma za Jamii, Utamaduni na Maendeleo. Mwaka 1990 - 1996 alikuwa Profesa kamili na Mkuu wa
Idara ya Kiswahili na Isimu katika Chuo Kikuu hicho cha Moi. Mwaka 1996 - 2000 alikuwa Profesa na Mkuu wa Idara ya Lugha, Isimu na Fasihi katika Chuo Kikuu
cha Kiislamu cha Mbale nchini Uganda. Baada ya hapo alifanya kazi tena kama Profesa na Mkuu wa Idara ya Lugha, Fasihi na Isimu katika Chuo Kikuu cha Moi.
Mwaka 2002/2003 alifanya kazi katika Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) kama Profesa kamili. Baadaye, mwaka 2003 akafundisha katika Chuo Kikuu cha Taifa cha
Zanzibar (SUZA) ambako alikuwa Mhadhiri na pia Mratibu wa Idara ya Utafiti. Alifanya kazi SUZA hadi mauti yalipomchukua tarehe 13/10/2012.
Mbali na kufundisha Almarhum Profesa Mohamed alikuwa mwandishi wa vitabu aliyebobea. Katika uhai wake aliweza kuandika vitabu kama vile:
Kipimo cha Mtihani - Utamaduni Publisher (1981), Ufahamu - Utamaduni Publisher, Fani za Sarufi - Foundation Publisher (1982), Review of Swahili Novels -
Press and Publicity Centre Ltd (1983), Ufupisho na Ufahamu - Press and Publicity Ltd, Sarufi Mpya - Foundation Publisher (197), Tahakiki Part I - Press and
Publicity Centre (1988), Tahakiki Part II - Press and Publicity (1989), New Summary for Secondary Schools - East African Publisher (1992), Kamusi ya Visawe -
East African Education Publisher (1996), Modern English Grammar - East African Education Publisher Ltd (2000), Kamusi Kuu ya Kiingereza - Kiswahili (Comprehesive
English - Swahili Dictionary) - East African Education Publisher Ltd, Kamusi Kuu ya Kiswahili - Kiingereza (Comprehesive Swahili - English Dictionary) -
East African Education Publisher Ltd. Aidha, Prof. Mohamed aliandika makala mbalimbali za kitaaluma katika majarida tafauti. Hadi anafariki alikuwa na niswada ya
Kamusi ya Vinyume (A Dictionary of Antonyms), Kamusi Fafanuzi ya Kiswahili na Swahili Encyclopedia.
Prof. Mohamed alichangia sana katika maendeleo ya taaluma ndani na nje ya nchi. Ingawa Profesa amefariki, juhudi aliyoifanya ya kufundisha kwa moyo safi na kutoa
machapisho kadhaa ni mambo ambayo yataendelea kumweka hai.
MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU PEPONI - AMIN