BAKIZA

BWANA SHAFI ADAM SHAFI

Mwandishi wa riwaya za Kiswahili zilizotafsiriwa kwa lugha za ughaibuni za Kirusi, Kijarumani na Kifaransa ni huyu anayejuilikana kwa jina la Shafi wakati wazazi wake walimwita kwa jina la Adam.


Tarehe 21 Juni mwaka 1940 ndiyo siku aliyokuja duniani. Uzawa wao wamezaliwa watoto tisa nao ni 1. Saad Shafi, 2. Rukia Shafi, 3. Arafa Shafi (Marehemu), 4. Adam Shafi, 5. Mohammed Shafi, 6. Salma Shafi (Marehemu), 7. Ali Shafi, 8. Zawadi Shafi, na 9. Fatma Shafi.


Adam amepitia madrasa na kusoma Kur' an kabla kupelekwa skuli. Kwa Zanzibar katika utoto na ujana wa Adam, elimu ya juu na taaluma ya heshima ilikuwa ni kusomea ualimu. Chuo kilichopo nje ya mji wa Zanzibar, pahala paitwapo Beit el Ras Adam alijiunga hapo mwaka 1957 baada ya kumaliza Skuli ya msingi na kuondoka mwaka 1960 kwa kuvutwa na shauku na hamu ya kupata elimu ya juu huko Ulaya. Misukosuko, shida, adha na tabu ya kuisaka elimu imekuwa moja ya hekaya za kazi zake za uandishi wa riwaya. Si haba, hatimaye jozi za nyayo zake zikazikanyaga na kuzikanyaga darzeni kadhaa za nchi za Ulaya na Ndoto Kutimu. Mwaka 1961 mpaka 1963 amekuwa Ujarumani Mashariki (GDR) na kuhitimu Diploma ya Siasa na Uchumi. Kiu ya kuisaka elimu haikuisha hapo hapo. Mwaka 1964 hadi 1965 amesomea uandishi wa habari ngazi ya Diploma huko Chekslovakia. Mwaka 1981 ameenda Sweden na mwaka 1982 ameenda Marekani kwa taaluma ya Habari. Kwa vile Ulaya aliendea moja na sio kumi na moja, baada ya kuipata elimu alirudi nyumbani na baada ya kuoa alibarikiwa kupata watoto wanne nao ni: 1. Riziki Adam Shafi, 2. Hawa Adam Shafi, 3. Shafi Adam Shafi, na 4. Laila Adam Shafi.


Mapema baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, Adam amekuwa mwandishi wa habari - kazi aliyoisomea. Mwandishi wa gazeti la Chama cha Wafanyakazi (FPTU) cha mrengo wa kushoto. Kati ya mwaka 1966 na 1974, Adam akawa mwandishi mkaazi wa magazeti ya Chama cha TANU cha Tanzania Bara yaitwayo "The Nationalist na Uhuru". Ajira hiyo ilikatishwa pale alipokamatwa na kusokomezwa korokoroni kwa tuhuma ya uhaini kwa miaka kadhaa kabla ya hukumu iliyomwengua kwa kukosa ushahidi kumnusuru. Adam ameacha taaluma ya habari na amejichovya katika riwaya bila ya kutarajiwa kama kupiga radi katika Kiangazi.

Riwaya zake za mwanzo ni "Kasri ya Mwinyi Fuad (1978)" inayoonesha harakati za kuuondosha umwinyi na usultan uliotamalaki. Mwaka mmoja baadaye 1979, aliandika juu ya wachukuzi wa bandarini kupitia riwaya ya Kuli. Mwaka 1999, aliibua riwaya ya mivutano ya kitamaduni ya Vuta N'kuvuta na Haini (2002). Hadi sasa, riwaya yake ya mwisho kutoka ni sharaja ya safari yake ya kwenda Ulaya iitwayo Mbali na Nyumbani.


Wakati tunasubiri kazi nyingine ya riwaya, riwaya zote zimejengwa kimaudhui na duwara la maisha ya mwandishi alokumbana nalo maishani. Nusu ya maisha yake ya miaka 37 ya ukubwani ameyatumia kuandika riwaya hizi za kimaendeleo ambazo zimempa umaarufu katika tasnia ya uandishi wa kazi za Fasihi.